All Kenyan should be behind your fellow.Deplore massive online campaign
..................................................................................
Waandishi Wetu
SERIKALI ya Kenya imesema inazifanyia kazi taarifa za raia wake
kukamatwa na kufikishwa kortini nchini kwa tuhuma za kumteka na kufanya
jaribio la kumuua Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven
Ulimboka.
Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Jeshi la Polisi kutangaza
kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa raia wa Kenya, Joshua Mulundi
anayetuhumiwa kuhusika na tukio la kumteka, kumpiga na kumtupa Dk
Ulimboka katika Pori la Akiba la Pande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam hivi karibuni.
Balozi wa Kenya nchini, Mutinda Mutiso, alisema kwa njia ya simu jijini
Dar es Salaam jana kuwa Serikali yake itachunguza uraia na tuhuma
zinazomkabili mtu huyo ili kubaini ukweli.
“Ndiyo kwanza nimewasili kutoka nje ya nchi…, nitafuatilia kwa makini
kupata taarifa sahihi kutoka kwenye vyanzo sahihi na mamlaka husika za
hapa Tanzania na Kenya ili kupata taarifa ya kweli,” alisema Balozi
Mutiso na kuongeza: “Siwezi kueleza zaidi kwa sasa kwani itakuwa naeleza
uvumi.”
MAT wadai kutoridhishwa
Wakati Balozi wa Kenya akisema hayo, Chama cha Madaktari Tanzania (MAT),
kimeelezea kutoridhishwa na hatua hiyo kikisisitiza msimamo wake wa
kutaka kuundwa kwa tume huru ya uchunguzi kwa lengo la kuwabaini
wahusika na kuchukuliwa hatua stahiki.
MAT pia imesema kwamba, inaendelea na mpango wake wa kuandamana,
ikibainisha kuwa kesho itawasilisha barua ya kuomba kibali cha kufanya
maandamano ya amani Polisi.
Imefafanua kuwa malengo ya maandamano hayo yaliyopigwa 'stop' na polisi
kwa kile walichoeleza ni sababu mbalimbali za kiusalama na kwamba, madai
mengi ya madaktari yamefanyiwa kazi na Serikali.
"Nisingependa kuingilia suala la kipolisi kwa ujumla wake, lakini moja
ya madai yetu ni kuundwa kwa tume huru ya kuchunguza tukio la kutekwa,
kupigwa na kutupwa katika Msitu wa Pande kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Madaktari Dk Ulimboka," Katibu Mkuu wa (MAT) Dk Rodrick Kabangila
aliliambia Mwananchi Jumapili jana.
TUCTA nao wamo
Katika hatua nyingine, Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi (Tucta)
limelipongeza Jeshi la Polisi kwa kumkamata mtu anayedaiwa kumteka na
kumpiga kiongozi wa mgomo wa madaktari, Dk Steven Ulimboka.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Tucta, Nicolaus
Mgaya alisema kuwa, hatua ya kumkamata mtuhumiwa huyo inaleta matumaini
ya kuwabaini watu wengine waliohusika na vitendo hivyo, jambo ambalo
linaweza kurahisisha uchunguzi.
Alisema kutokana na hali hiyo, jeshi hilo linatakiwa kuendelea na
uchunguzi ili waweze kuwabaini wahusika wengine na kubaini ukweli kuhusu
tukio hilo ambalo limesababisha kutokea kwa hisia tofauti katika jamii.
“Tunaliomba Jeshi la Polisi liendelee na uchunguzi ili waweze kuwabaini
watuhumiwa wengine na kuwachukulia hatua za kisheria,” alisema Mgaya.
Mkenya kukamatwa
Joshua Mulundi, ambaye anatuhumiwa kumteka na kumtesa Dk Ulimboka
alikamatwa na kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu jijini Dar es Salaam juzi alasiri na kusomewa mashtaka mawili na
Wakili wa Serikali, Ladslaus Komanya.
Wakili Komanya alidai mahakamani hapo kuwa, Mulundi ambaye makazi yake
ni Murang'a nchini Kenya mnamo Juni 26, mwaka huu akiwa eneo la Leaders
Club alimteka Dk Ulimboka.
Hata hivyo, kumetokea utata wa jina, umri wake na makazi ya mtuhumiwa huyo.
Wakati hati ya mashtaka mahakamani inasema ni Joshua Mulundi mwenye umri
wa miaka 21, mkazi wa Murang’a nchini Kenya, taarifa ya Jeshi la Polisi
imesema anaitwa Joshua Mahindi mwenye miaka 31 na mkazi wa Namanga
nchini Kenya.
Katika shtaka la pili, Wakili Komanya alidai kuwa tarehe hiyohiyo
mshtakiwa alifanya jaribio la kumsababishia kifo Dk Ulimboka kwa kumpiga
katika eneo la Msitu wa Pande eneo la Tegeta jijini Dar es Salaam,
kinyume cha sheria.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo alikana mashtaka hayo akidai kuwa makosa aliyoshtakiwa nayo siyo sahihi.
Hakimu Mkazi, Agnes Mchome alimwambia kuwa hatakiwi kujibu chochote kwa
kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo, isipokuwa
Mahakama Kuu pekee.
Afya ya Dk Ulimboka yazidi kuimarika
Akizungumzia hali ya Afya ya Dk Ulimboka anayeendelea na matibabu nchini
Afrika Kusini, Katibu Mkuu huyo wa MAT alisema kuwa, Mwenyekiti huyo wa
Jumuiya ya Madaktari Tanzania anaendelea vizuri na sasa ameanza kufanya
mazoezi ya kutembea.
"Taarifa tulizonazo sasa ni kwamba, hali ya Dk Ulimboka inaendelea
vizuri. Ameanza kufanya mazoezi ya kutembea mwenyewe, anakula na pia
anaweza kuzungumza vizuri. Amekuwa akifanya mawasiliano yeye mwenyewe na
madaktari wenzake wa hapa nchini ingawa bado kuna matibabu anayoendelea
nayo," alisema Dk Kabangila.
Mmoja wa Madaktari wa karibu wa Dk Ulimboka aliyepo nchini, alisema
Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania amewatumia ujumbe wa
kuwashukuru wanataaluma wenzake na Watanzania wote waliomchangia na
kumwezesha kupata matibabu nchini humo.
Hata hivyo alisema kuwa, Dk Ulimboka ameomba suala la tukio lake la
kutekwa na kuumizwa lisiwe hoja ya kujadili, badala yake madaktari na
wananchi wote wajielekeze kudai haki zao, ambazo Serikali haijazipa
kipaumbele.
Dk Ulimboka alisafirishwa nje ya nchi Juni 30 kwa ajili ya matibabu
kufuatia jopo la madaktari lililokuwa likimtibu likiongozwa na Profesa
Joseph Kahamba kudai afya yake imebadilika ghafla na pia angestahili
kupelekwa nje ya nchi kwa ajili ya vipimo na matibabu zaidi ambayo
hayapatikani hapa nchini.